Kila mtu anatumia fedha, sisi sote
tunataka fedha na tunafanya kazi kutafuta pesa zaidi na mara nyingi tunafikiri
juu ya fedha na matumizi yake. Hebu fikiria kama kungekuwa hakuna fedha duniani
maisha yangekuwaje leo. Hebu fikiria umefika dukani na unataka kununua kitu
lakini mfukoni huna fedha ya aina yoyote ungefanya nini? Labda ungeweza
kumuomba mwenye duka akupe kazi ya kupanga mabox na ufanye usafi dukani ili akupe
kilo moja ya mchele. Fedha ina kazi kubwa mbili:-
(1)
Ni kitu ambacho kinakuwezesha kubadilishana na mtu mwingine vitu au
huduma kama vile kununua chakula au muda wa maongezi kwa simu yako.
(2)
Ni ghala la thamani, fedha inakuhifadhia thamani ambayo unaweza kuitumia
baadae utakapohitaji kitu au huduma fulani ambayo itasaidia katika kukufanya
ufurahie maisha yako.
Fedha hainunui penzi lakini penzi
haliwezi kununua zawadi ya valentine, fedha haziwezi kununua penzi lakini
hurahisisha kazi ya kupendana sikiliza kesi hii.
Mimi ni dada wa miaka 27 nimekuwa na
uhusiano na kaka mwenye uwezo mkubwa wa kifedha kwa zaidi ya mwaka mmoja la
ajabu ni kwamba anajipendelea sana yeye mwenyeywe na haangalii kipato change
kidogo, atanunua simu mpya, laptop mpya japo anazo za zamani zinazofanya kazi
na kwa upande wa nguo usiseme makabati hayatoshi. Inaniumiza kuona anaishi
maisha ya fahari na haoni ninavyohangaika. Naogopa kuzungumza nae juu ya hilo
kuogopa kuonekana napenda pesa zake zaidi na inaniumiza moyo wangu.
Ningependa nitoe angalizo kwa wanaume
ambao wana wapenzi ambao wana uwezo mkubwa wa kifedha zaidi yao. Kwa mwanaume
ni muhimu ukumbuke kuwa haijalishi mwanamke ana uwezo mkubwa wa kifedha kiasi
gani angependa aendelee kuchukuliwa kama mwanamke na unapaswa kuhakikisha kuwa
unampa mahaba sahihi na ya kutosha nje na ndani ya chumba cha kulala. Onyesha
shukrani za kutosha juu ya mchango wake mkubwa kifedha japokuwa mwanamke huyo
ana uwezo mkubwa kifedha. Kumbuka kuwa mwanamke huyo bado anatarajia
zawadi utakayomchagulia wewe kuonyesha jinsi gani unamuona ni wa kipekee.Kwa
kufanya hivyo utamzuia asione uwezo wako mdogo wa kifedha kutokana na ukubwa wa
penzi lako.
Mwanamke ambaye anajikuta ana fedha
nyingi kuliko mwanaume ajitahidi kuepuka kuonekana yeye ndie dereva wa uhusiano
wao, tambua mwanaume hatavumilia aina yoyote ya dharau au kupewa nafasi ya
chini kwako. Hivyo kuwa mwangalifu katika maneno na mwenendo wako. Kama
mwanamke lazima ukumbuke kuwa mpenzi wako angependa akulipie huduma fulani
japokuwa uwezo wake wa kifedha ni mdogo hivyo aonyeshapo nia ya kufanya hivyo
usimzuie.
Mwisho kwa wote wawili pale mnapotoka
kwenda hotelini kwa chakula na vinywaji ni muhimu mjadiliane kuwa ni nani
atakaelipa ili isijetokea hali itakayomuaibisha yule mwenye kipato kidogo
na kuleta maumivu kwake.
Wataalamu wa sayansi ya mapenzi katika
tafiti zao wanasema asilimia 35 ya wapendanao hugombana juu ya mambo yanayohusu
fedha kila wiki na asilimia 10 ya wapendanao hukwazana juu ya mambo yanayohusu
pesa karibu kila siku. Takwimu hizo zinakupa mwanga juu ya umuhimu wa kuangalia
kwa makini juu ya eneo hili. Na kama takwimu hizo tungezibadilisha sura yake
itatutisha na kuweza kufanya bidii katika mwenendo wetu juu ya pesa na tukasema
asilimia 35 ya wapendanao huachana kila wiki kutokana na mambo ya pesa bado
tungekuwa tunasema ukweli kwa asilimia fulani kwani ni kweli kwamba wapo watu
ambao wameharibu ndoa zao kwa sababu ya pesa kidogo kuwepo kati yao au kuwepo
kwa pesa kupita kiasi na mgogoro ukazuka juu ya nani atumie nyingi zaidi ya
mwenzie na zitumikeje pesa hizo. Mara nyingi kutokana na kushindwa kupanga
matumizi mazuri ya fedha watu wengine wamejikuta wakinunua penzi nje ya ndoa
zao kuziba mapungufu yaliyomo katika ndoa zao.
Tafiti ya hivi karibuni inasema kuwa ni
rahisi kutabiri ndoa itakayovunjika uonapo mke na mume ambao hawaelewani au
kugombana katika mambo yanayohusisha fedha. Kiongozi wa utafiti huo Dr. Jeffrey
Dew anasema kwa kuwa kila mtu ana mtazamo wake juu ya maeneo muhimu ya matumizi
ya fedha .Na kutokana na umuhimu wa fedha katika maisha yetu ni rahisi
sana watu kushindwa kuelewana katika eneo hilo. Mshiriki mwingine katika
utafiti huo Dr. Sonya Britt anasema sio tendo la ndoa, watoto au wakwe
vinavyoongoza katika kuleta msukumo wa watu kuachana bali ni fedha na mambo
yahusuyo fedha. Kwa wanaume imeonekana kuwa walijikuta wanataka kuachana na
kuvunja ndoa juu ya masuala yahusuyo fedha pekee na kwa wanawake ilikuwa
masuala ya fedha na tendo la ndoa jambo linalothibitisha hali ya wanawake
walioolewa na wanaume wenye fedha nyingi kwenda nje ya ndoa. Pamoja na hayo
bado ilionekana ili kuwa pale inapotokea ugomvi juu ya pesa watu hutumia maneno
makali zaidi kuliko katika maeneo mengine. Jambo linaloweza kutengeneza uhasama
kati ya wapendanao. Dr Jeffrey Dew anasema kuwa utafiti wao unaonyesha hoja ya
wapendanao kutumia akili yao vizuri katika mambo yahusuyo fedha na umuhimu wa
kukagua hisia na mitazamo tuliyonayo juu ya fedha na matumizi yake.
Labda nitoe mifano michache
hapa,mwanaume anaombwa fedha ya maziwa ya mtoto wao wa mwaka mmoja na kwa kuwa
anajua mke wake anafanya kazi anasema hana fedha akijua maziwa hayatakosekana
kwani mke wake anao uwezo wa kununua.Inatokea jioni hiyo hiyo mwanaume huyo
anaona watembeza viatu ananunua viatu vizuri sana ,je hapo mwanamke
hatakasirika?Akikasirika na hasemi kitu na hapohapo sayansi inasema wanawake
wengine wakikasirika hupatwa na hamu ya tendo la ndoa na mwanamke huyo
akivamiwana hamu ya tendo la ndoa na akakumbuka JOHN alikuwa anamtaka kwa muda
mrefu si ataenda kwa JOHN na kumpa kuchikuchi? usaliti una vyanzo
vingi na pesa inaweza kuwa kianzishi.Na angalia mwanamke anaemwambia mchumba
wake kuwa hana pesa kabisa na anaomba msaada kwa mchumba wake lakini baadae
anaonekana na gauni jipya kabisa na ni la bei mbaya huoni mchumba wake
atafikiria vibaya? kuna mambo mengi yanayofanana na hayo kama vile mwenzio
anakuomnba fedha na ukasema huna na akatokea ndugu yako akakuomba pesa ukampa
hayo yote huleta maumivu makali kwani mtu anajiona kuwa hapendwi.
Ni kweli kuwa fedha haziwezi kununua
penzi lakini huwezi kusema kuwa fedha sio muhimu katika ujenzi wa penzi. Katika
historia ya wanadamu imeonekana wazi kuwa mara nyingi ukiwa na uwezo mkubwa wa
kifedha imesaida mtu kupendwa na wengi zaidi. Ni vigumu kwa mtu kukubali kuwa
hatojali kuwa na mtu asiekuwa na pesa lakini wengi wangefurahia kuwepo na pesa
za kutosha katika penzi lao.
Utafiti uliofanyika na Chuo kikuu cha
TEXAS huko Marekani unaonyesha kuwa kupungua kwa fedha katika uhusiano ulioanza
katika mazingira ya kuwepo pesa nyingi husababisha watu wawili waliopendana
kipindi cha kwanza kuachana kutokana na pesa kupungua. Hivyo inatokana kuwa
pale ambapo inaonekana kuwa fedha hazitoshi kwa mahitaji yaliozoeleka au
mahitaji yanayotamaniwa mikwaruzano kati ya watu wawili wapendanao huongezeka
na kusababisha kutoridhika na uhusiano huo.Kutoridhika huko kutasababisha
mikwaruzano na usaliti wa chini kwa chini.
Daktari mwingine aliefanya utafiti
katika eneo Dr. Terri Orbuch anasema haijalishi watu wanapendana kiasi gani
marumbano yanayohusu pesa hutingisha sana mahusinao hayo. Tafiti hiyo ya muda
mrefu inaonyesha kuwa katika ndoa 10 ndoa 7 lazima zitakuwa na mizozo na
mvutano katika eneo hilo na Dr. Terri anasema ndio maana watu wengi hukwepa
kuzungumzia hisia zao juu ya jambo hilo. Pamoja na hilo pia imeonekana kutokana
na ugumu wa kuzungumzia hisia za mtu juu ya swala hilo mtu anajikuta anamchukia
mwenzie bila kumweleza kwani anamuona kama mzigo au anaona anatumiwa kama ATM
ya Benki.
Haijalishi mtu ana fedha nyingi kiasi
gani lazima atakuwa anafikiria juu ya kupungua na kuongezeka kwa fedha zake na
zaidi ya hayo angependelea kuwa fedha zake zinaongezeka hivyo atokeapo
mtu ambae anasababisha zipungue lazima ataonekana kama tishio kwake.Hofu ya
kupungua kwa fedha na aibu ya kutokuwa na fedha za kutosha zitasababisha
misuguano ya hapa na pale.
Hisia juu ya fedha unaweza kuziona
zinajitokeza kama ifuatavyo, iwapo unaogopa kuishiwa fedha hapo hapo unakuwa
unaogopa kudharauliwa na kuachwa na hivyo hatua zako za kutaka kujilinda na
hayo lazima zitaleta migongano.
Iwapo unajikuta huna fedha za kutosha
kukidhi mahitaji ya mpenzi wako unajiona kuwa hufai kwani humtoshelezi mahitaji
yake, hali hiyo huleta uchungu nafsini. Kwa kuwa hupendi uchungu huo ujulikana
utajikuta unajawa na hasira wakati wowote pale fedha inapohitajika kwa matumizi
Fulani na hasira hiyo italeta chachu kati yenu.
Utafiti uliofanywa na gazeti moja la
SELF magazini miongoni mwa wanandoa 23,000 ilionekana kuwa asilimia 40 yao
walisema uongo juu ya matumizi ya fedha zao. Kati ya wanandoa hao
asilimia 60 wanasema kuwa kushindwa kuwa mwaminifu kwenye matumizi ya fedha ni
sawa na mtu kushindwa kuwa mwaminifu na kufanya mapenzi nje ya ndoa. Na kati ya
watu hao 1/3 wamesema kuwa kutokuwa mwaminifu katika matumizi ya fedha humfanya
mtu kuhalalisha uzinzi nje ya ndoa.
Fedha hazifanyi kazi ya kununua vitu au
huduma peke yake, pesa zinaweza kusaidia mtu kuoneysha mapenzi, ubabe na uhuru
pia jinsi gani mtu anapenda pesa zake zitumike ni uamuzi wake binafsi na hivyo
pale ambapo mtu mwingine ana shiriki matumizi ya pesa zake uhuru wake kwa
kutumia fedha hizo unaingiliwa na hivyo kama penzi la watu wawili halina mizizi
mizito lazima mvutano wa aina fulani utatokea na isipotumika hekima migogoro
itachipua kwa urahisi.
Kwa mfano mpenzi wako anaomba
umtumie shilingi 20,000 na yeye hajui umepangia nini fedha zako na wewe ili
usionekana huna pesa unatoa kwa shingo upande. Angalia hivi juzi umempa
shilingi 20,000 leo unamwambia aje alale kwako unatoa visingizio hali
hazuiliwi na wazazi au mtu yeyote. Sisemi kuwa kwa kutoa shilingi 20,000
ndio amenunua penzi na lazima alipwe nasema angalia hisia za mtu huyu, na mfano
huo huo ukigeuza utaona jinsi gani migogoro hutokea.
Ugeuze hivi leo mchumba wako wa kike
kwa hiari yake mwenyewe kajitolea kuja kulala kwako akisema ana hamu na wewe na
wewe ukafurahi sana lakini siku tatu zijazo akakuomba Tshs. 20,000 ulioipangia
jambo fulani muhimu na ukamwambia sina dada huyo ataumia sana kwani anaona
humpendi. Na kama utatoa pesa hiyo kwa shingo upande tayari umeathirika
kisaikolojia.
Shida iliopo inatokana mtazamo wa mambo
ya kifedha kati yenu. Unaweza kuona mtu analipia chakula hotel, chumba na hata
kukupa hela ya nauli lakini ukimuomba Tshs 20,000 akakunyima unaona hakujali
kikamilifu. Huoni kiasi gani anatumia kwa starehe zenu na
mawasiliano yenu pia hujui mipango mikubwa aliyonayo. Hebu angalia mfano huu
huyu dada kabla hajapata kazi mchumba wake alijitolea gharama zake zote za
saluni na chumba anachoishi na sasa dada huyo amepata kazi bado anataka mchumba
wake aendelee kumlipia chumba alichopanga na gharama za saluni eti kw akuwa
kaka huyo ana kipato kikubwa.